Ni Siri Kuu - The Great Mystery

Ni Siri Kuu - The Great Mystery
"Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.

Alhamisi, 7 Aprili 2016

JIJENGEE MTAZAMO SAHIHI ULIYE MKRISTO WA SASA


Mwl; Goodluck Kazili

KUMUHUSU MUNGU
Ni kweli kuwa kila mtu ana mtazamo wake kumhusu Mungu, tena kila mtu kuna jinsi anavyoamini juu ya Mungu kuhusu mambo mbalimbali ya kimaisha. Na hili ndilo jambo kuu ambalo unapaswa kulitazama kwa upya, mtazamo ulio nao juu ya Mungu kuhusu maisha.
Ni kweli kuwa kila mtu kuna maisha aliyoandikiwa tena aliyokusudiwa kuishi, maana kwa vyovyote vile lazima aliyekuumba kuna maisha aliyokukusudia, na hayo maisha kwako ni ya muhimu kuliko hata yale unayoyatamani.
Swali rahisi la kujiuliza ni hili, kama wewe ingekuwa ndiye uliyeumba, na hivyo ulivyoviumba vyote umevipangia maisha , je ungeviacha viishi hayo vinayoyataka au ungevilazimisha viishi yale unayoyataka?. Kama hiyo haitoshi, vipi kama yale maisha vinayoyataka haviwezi kuyapata, kisha vinakuja mbele yako kukuomba ambako ni kama kukulazimisha uvipe maisha vinayotaka mbali na yale wewe uliyoyataka viishi, je! utavijibu na kuvipa hayo maisha vinayotaka au utanyamanza ili vikose yote?
Hii ndiyo hali ambayo Mungu wetu anakutana nayo; maana kwa hakika alituumba/alikuumba na kwa namna yoyote ile kuna maisha aliyoyakusudia wewe uyaishi, lakini sisi/wewe kuna maisha ambayo unayataka kuyaishi ambayo kwa namna flani si yale ambayo Yeye anataka uishi. Na uzuri ni kuwa wewe huwezi kujifanikisha kuishi hayo maisha unayoyataka, ambapo inakulazimu kuomba msaada kwake ili akusaidie uishi maisha hayo unayoyataka na siyo yale ambayo Yeye anataka na amekupangia.
Ugumu huo umempata Mungu, kwa miaka mingi, tangu hapo mwanzo alipomuumba mtu wa kwanza, ijapokuwa wako waliotafuta maisha ambayo anapenda na anataka waishi, lakini wengi wao waliishi yale ambayo wao wanataka na wanaona yanafaa. Hivyo aliwaangamiza kwa hasira kwa kuwa asema “Nafsi yangu haitashinda na mtu kamwe”.
Jifikri kidogo maisha unayoyataka, je! Ndiyo ambayo Mungu wako anayataka uishi?, na je ndiyo yatakayoupendeza moyo wake?, maana hakukufanya ili ahuzunike bali akufurahie kwa kuishi maisha yenye heshima na utukufu kwake. Lakini hakuna anayefikri hayo, kila mtu amegeukia njia zake za maisha, na ikiwa haitoshi humuomba kila siku awafanikishe katika maisha hayo wayatakayo. Na kwa sababu hiyo, naye ameamua kunyamanza na kuwaacha kila mtu aiendee njia yake aionaye inafaa  katika maisha.
Ni wazi kuwa Mungu hajawasukumia mbali watu wake, lakini pia hayuko karibu na watu wake, kwa kuwa haiwezekanai kuwa karibu nao wasipoishi maisha anayoyataka wayaishi.
Lakini pia hawasukumii mabali kwa kuwa anawapenda ijapokuwa wanajipotosha nafsi zao kwa kuziendea njia zao wenyewe.
Ni wazi kuwa shauku ya Mungu kwetu, ni kila jambo, kila kitu, kipitachao katika maisha yetu kimletee heshima na utukufu Yeye. Na kwa maana hiyo, aliifanya nafsi iliyo kwa namna yake na kuipa uwezo wa kutawala, ili katika kutawala huko Yeye ajipatie heshima. Lakini kinyume chake amehuzunishwa sana  na hizo nafsi alizozifanya, kwa kuwa tu hazitimizi ile adhima yake aliyoikusudia katika kuzifanya kwake.
Ndugu katika Kristo Yesu, Bwana anakutaka leo ufikri jambo hili, je! Hayo maisha ulionayo, na unayoyatafuta na kumuomba kila wakati ndiyo maisha aliyoyakusudia na anayoyataka kutoka kwako?, tafakari vema uone utakalofanya, maana ijapokuwa hatakujibu katika hayo unayomuuomba lakini pia atajilipa kwa wakati aliouamru, kwa hivyo, ni heri kwako kama leo utajifkri upya juu ya Mungu wako kuhusu maisha yako.
Si kwamba anashindwa kukupa maisha hayo unayotaka , maana wote twajua kuwa kila kitu ni kazi ya neno lake tena ni kazi ya mikono yake, na vyote vimetiishwa jini ya mbingu zake na ameifunga amri ya kuihusu hii inchi katika mbingu hizo, na lolote analoamuru ndilo linalokuwa, sasa je ! kashindwa kukufanikisha kuhusu hayo unayomuuomba kila siku?, au liko tatizo gani hadi asikufanikishe? Hakika yake nayashuhudia haya katika Roho Wake Mtakaifu, kuwa ni kwa kuwa hayo unayoyaomba mengi yake siyo yale aliyoyapanga wala anayoyakusudia kwako, maana yako maisha anayoyatamani kutoka kwako, na aliyo yapanga. Hivyo hawezi kukupa yale unayoyataka wewe ikiwa wewe hutaki kutafuta yale ya kwake ambayo ameyakusudia na anayataka wewe uyaishi.
Hivyo, unao uchaguzi pia, wa kuendelea kujibidisha katika hayo yaliyo ya shauku yako, au kujifikri upya na kubainisha iliyo kweli yake kwako, na kujitia katika kujua anayoyataka kwako, na kuanza kuyaishi na kumuomba katika hayo kwanza, ili ukishafanya na kuishi hayo ayatakayo, katika hali hiyo nawe waweza kumuomba yale uyatakayo, kama ni ya kufaa, hakika yake atakupa na kukuzidisha zaidi ya hayo utakayoomba.
Lakini ikiwa utajibidisha katika hayo unayoyatamani, basi hakika yake utayakosa yote, maana Mungu si dharimu wala habahatishi, kiasi cha kufanya jambo lisilo maana, kwa kuwa kila kitu amekifanya kwa kusudi, tena katika kila kazi aliyoifanya aliikusudia imletee heshima na utukufu, hivyo kusudi hilo haliendi bure. Ikiwa wewe uliyemhusika hutataka kulitimiza, basi hakika yake ni kuwa hata wewe hautafanikiwa katika hayo unayoyatafuta na kumuomba kila siku, tena ijapokuwa aweza kukuacha ukafanikiwa katika hayo lakini bado atakukondesha roho/nafsi yako, na haitakuwa na raha, tena atakuhukumu kwa siku ile aliyoiweka kuzihukumu nafsi zote za wanadamu.
Ndugu nakuhimiza na kukusihi katika Kristo, kuona kuwa imetosha, kumtia Mungu wetu katika hali ya kutokutufurahia, maana asema “ nafsi yangu ingezimia kwa hizo nafsi nilizozifanya” kwa nini kumtia Mungu wetu katika uchungu kwa nafsi zetu. Je! gharama aliyoingia ya kutukomboa katika uteka ambao tusingeweza kujitoa haitoshi sisi kufkri? Tena ikiwa hiyo haitoshi ya kutukombao akatupa nguvu na kutupa urithi wa yale tuliyokuwa hatusitahili tena kuyarithi kwa jinsi tulivyokuwa tumeasi, lakini kwa pendo na neeama tena na rehema zake akatukirimia nafasi hiyo tena.  Je! Si ingekuwa heri leo kama ukiyatia haya katika moyo wako na kuyafkri kwa kina,  tena kuchukua hatua ya kumwendee Yeye na kutaka kwake kujua maisha anayoyataka kwako, ili sasa upate kuyaishi na kuifurahisha Nafsi yake?. Maana hakuna jambo lililo kubwa kwake zaidi ya nafsi yako kuhudhulia mbele zake na kumfanyia ibada.
Lakini je! nafsi ya mtu ikiwa yasema yampenda Mungu, na huku wajibidisha katika mambo yako na yale uyatakayo na kuyaona kuwa yanafaa,
 je! Mungu ataifurahia nafsi hiyo, maana nafsi ya Mtu ndicho kitu pekee kinachoweza kumfurahisha Mungu, ikiwa tu kitahudhulia mbele yake na kumuabudu na kumpa utukufu.
 Kadhalika kitu pekee kinachoweza kumkasirisha Mungu sana ni nfasi ya mtu kutokuhudhulia mbele yake na kufanya ibada, tena kutokumpa utukufu Yeye anayestahili ambaye aliiumba nafsi ili ifanye hayo.
Ni kweli kuwa maisha pia yana namna ya mwili, ambayo ina uhitaji mkubwa tu wa vitu mbalimbali, ambavyo hivyo vyatukimbiza sana. Je! kwani aliyeumba hakujua kuwa hayo yote tunayahitaji, au ni nani aliyeyaweka hayo?  je! kuna mtu aliyejiamuru kula, kuna mtu aliyefanya hitaji lolote katika mwili wake, si Mungu aliyeyaweka yote? Na ikiwa Yeye ndiye aliyeyaweka yote, basi kwa hakika kwa kila maisha aliyoyapanga basi ameweka pia mahitaji hayo katika utimilifu wake. Maana dunia nzima iliumbbwa kwa ajili ya matumizi ya huo mwili, maana alipoipanda bustani ya edeni hayo yalikuwa mahitaji ya mwili, tena alimuwekea uzuri wa kila namna maana Yeye kama Muumbaji alijua tena anajua mahitaji ya hicho alichokiumba kwa kuwa kila lionekanalo kuwa hitaji Yeye ndiye aliyeliweka ndani ya huyo mtu.
Kwa kuwa huo ndio ukweli ulio halisi, je! Ni sawa kujisumbua katika hayo hadi kumsahau Yeye? Na hata tunapomukumbuka, tunamukumbuka kwa kutaka atusaidie na kufanya hayo ambayo tunayataka?. Ikiwa iko hivyo, maana na tafsiri ya hayo, ni kuwa tunamlazimisha afanye, maana ikiwa Yeye ametutaka tuishi maisha flani, nasi twataka mengine na kuenda kwake kwa kuomba afanye vile tutakavyo, hilo humaanisha kuwa twamlazimisha. Na kwa jinsi mashauri yake yasivyopingika, twajikosesha wenyewe na kujilemea, maana ni afadhali yetu kama tungejitia chini ya kongwa lake na kuyataka hayo maisha ayatakayo sisi tuishi, ingekuwa salama na amani kwetu.
Maana tujapojibidisha katika hayo, hakika hatutayapata, na hata kama tutayapata hakika tutaangamia. Ya nini kuyakosa yote, tena ya nini kuangamia katika mambo ambayo tulipewa lakini tu twashinda kufuata utaratibu wa Yeye aliyetufanya na kuviumba vitu vyote.
Katika hayo yote, ujumbe huu hauwezi kwenda bure! Maana ikiwa Roho wake ajibidisha kututia katika kweli yote, ili kusudi nasi tulio kuwa tumesukumiwa mbali, tena watu tusiomjua Mungu, wala kuwa na ushirika nae, kwa nini nafasi hii tusiyoitafuta, tusiitumie vizuri? Maana ijapokuwa twaubatilisha ukweli, lakini iko wazi kuwa sisi tu watu tu, tuliopata neema maana hapo kwanza hatukusitahili, hata kumkaribia Mungu, wala hakuna maisha yaliyoamriwa kwetu dhahili ambayo tungeweza hata kujibidisha na kuyapata. Lakini kwa jinsi wema wake na pendo lilivyokuwa kuu kwetu, lilimbidisha hata kujitoa nafsi yake kuyakabili mauti naam mauti ya msalaba ili tulio mbali tuletwe karibu, tena tusioweza kukaribia mahali pake tukaribie ili tumletee heshima na utukufu anaostahili kwa hiyo kazi yake.
Twajikosesha sana, kutokujibidihsa katika mapenzi yake, na hayo maisha anayoyataka kwetu, maana haya tuyatafutayo ni ubatili, tena usiofaa kitu katika ulimwengu huu wala ule ujao. Inafaa nini tena, katika haya maisha yako, je! Si kujisogeza kwake kila wakati na kumpa heshima na utukufu, kwa kuimimina nafsi yako mbele zake na kumuandama Yeye katika mambo yote. Maana asemapo “nami nitawapa raha nafsini mwenu”, ni hakika kuwa ni kwa kujibidisha katika kumtafuta Yeye ili nafsi yako ipate hiyo raha.
Haizuiliwi kutafuta mahitaji yako katika mwili, lakini haifai kuyatafuta yale yaliyo nje ya mapenzi yake, yale yaliyo nje ya anayoyataka kwako. Maana ni hakika kuwa Yeye apenda ufanikiwe sana, lakini si nje ya yale ayatakayo kwako. Ikiwa unaweza kuyajua hayo ayatakayo basi wewe utakuwa aliyefanikiwa sana, maana ijapokuwa tunahitaji sana, lakini tusiyoyajua kuwa tunayahitaji ni mengi tena ndiyo yenye maana sana kuliko hayo.
Mwenyewe amebainisha wazi kuwa “ mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” tena “itamfaidia nini mtu akiupata ulimwengu na mambo yake yote lakini akapata hasara ya nafsi yake?” yafkri hayo kwa undani ujue hakika yake, maana ikiwa nafsi yako haitaokoka mpaka mwisho, basi ni heri usingelizaliwa.
Maana ijapokuwa haiwezekani kuupata ulimwengu wote na mamabo yake yote, lakini asema hata kama ingekuwa hivyo, bado thamani yake hailingani na nafsi yako. Je ikiwa hayo yangetiwa moyoni mwako leo, utaendelea kujibidisha sana katika mambo hayo ya ulimwengu ikiwa hujajihakiki nafsi yako kuwa salama? Maana kuangamia kwa nafsi ni ile kutokuwa na uhusiano mwema na Mungu, tena kutokutimiza Yale ambayo nafsi hiyo imeaandikiwa.
Pamoja na mambo yote, haitafaa lolote kama nafsi yako haitafika mwisho mzuri, maana ijapokuwa mbingu na nchi zitatoweshwa lakini nafsi yako haitapita kamwe, hata itakapotelemshwa kwenye mauti au kuingizwa katika mbingu mpya na nchi mpya. Maana twajua hakika kuwa, nafsi ya mtu haitapata kifo hiki tukijuacho katika mwili, maana kinachokufa ni mwili na siyo nafsi. Maana kipo kifo ambacho hicho huuhusu mwili, lakini pia yako mauti ambayo hayo huihusu nafsi. Maana kuna tofauti kati ya mauti na kifo, kwa kuwa kifo ni kwa ajili ya mwili na mauti ni kwa ajili ya nafsi. Mauti ni mateso na maumivu, wakati kifo huhusu mwisho wa uhai.
Yafikri haya sawasawa, maana ikiwa Roho Mtakatifu amekushirikisha wewe,  hailengi mwili wako hata kidogo, maana mwili unaweza kuyadharau wala usione kuwa kitu cah kufaa, lakini mambo haya yanailenga nafsi yako ambayo ndiyo yenye thamani kuliko vitu vyote, maana katika haya nafsi yako, itafunguka, na kujua uhalisia wake.
Maana asema “ nia ya mwili ni mauti lakini nia ya roho/nafsi ni uzima na amani”, je! Mwili huo utayafikri haya na kuyabaini au utayaona kuwa kitu? Ingekuwa heri kama nafsi yako itapambazuka na kuyafikri haya, ili kujitia ufahamu katika Roho Mtakatifu, uliyeshirikishwa.
Hata hivyo, Mungu ni mwaminifu kwa watu wake, maana walio wake awajua, na tena waisikia sauti yake, hao ndio walioitwa na Yeye katika wito wa msalaba, akawakaribisha kwake kwa kuwa walipoitwa waliitika, nao walitamani kukombolewa kwa kuwa walichoshwa na uteka waliokuwa nao. Ikiwa Mungu wa mbinguni amekupa neema hiyo, ni hakika kuwa haya utayatia katika moyo wako na kuyaamua vema kwa ajili ya utukufu wake Mwenyewe, ila kwa njia hiyo upate kujibidisha katika kuhudhulia mbele zake, ili ayamimine mapenzi yake ndani ya nafsi yako na upate kufanana naye na kumfaa zaidi kwa kila neno, tendo na uwazalo.
Katika yote, Roho wake Mtakatifu, ajifunue wazi, na kuyathibitisha yaliyo mapenzi ya Baba, katika Mwana, ili nasi tulio nafsi zake, tupate kuyapokea na kujitia katika kweli yake yote.
Hata hivyo yafaa sana ukiyafikri na kuyabaaini haya, ambayo kwa hakika yanafaa sana, na ni kweli itokayo kwa Mungu ambayo kwa Neema ya Kristo, Roho wake Mtakatifu ametushirikisha. Kama alivyoyamimina ndani yangu, nami nayapokea kutoka kwake, na kumlilia sana anisaidie niweze kuyatia katika fahamu zangu na kuyatekeleza bila upungufu wowote. Mambo haya ni matamu sana, tena yanatia uchungu sana kwa kuwa, kwa hakika huyo Mungu wetu ni wa ajabu sana, tujapomfikri katika hayo hakika hatutamuelewa wazi jinsi alivyotufadhili na kutupenda.

Mwl; Goodluck Kazili
0765 129 960
kazili.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni


Kunihusu

Picha yangu
"Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, baba , kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. (Ni Siri Kuu)

Tafuta katika Blogu Hii