Ni Siri Kuu - The Great Mystery

Ni Siri Kuu - The Great Mystery
"Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.

Ijumaa, 13 Machi 2015

Taarifa ya huduma ya KGT iliyoifanya Galigali na msukumo Wa timu

01. UTANGULIZI

Hii ni Taarifa ya KUHANI GOSPEL TEAM (KGT) juu ya huduma ya kiroho iliyofanyika Galigali, huduma ilifanyika tarehe 7/09 hadi 14/09/2014. Katika huduma hii timu ya watu 30 walishiriki, 17 wakitokea Mpwapwa na 13 wakitokea Dodoma mjini. Huduma kubwa iliyofanyika ni ya uinjilist wa kitongoji kwa kitongoji, shamba kwa shamba, nyumba kwa nyumba pamoja na mkutano. 

02 GALIGALI YENYEWE
  
02.1 KIUTAWALA/KISELIKALI
Galigali inaundwa na maeneo/vitongoji karibu 7 ikiwemo Izumbawanu, Mlowa, Mfilo, Iwanginyi, Ngh’uluwe, Dibulilo na kakwandali. Inakadiliwa kuwa na wakazi zaidi ya 3000 na kaya zaidi ya 600.

02.2 KIJOGORAFIA
 kijogorafia galigali iko mlimani, kuna umbali wa Km 20 kutoka mbuga, imezungukwa na vijiji kama  mbuga, lufu, makosa, makoleko, chogora, kikuyu na matonya. Ina vitongoji 7 na imezungukwa na milima mikubwa inayofanya miundombinu ya Barabara na mawasiliano kuwa magumu. Hali ya hewa ni nzuri kwa kilimo, imezungukwa na misitu na milima inayofanya nvua kuwa nyingi, inakadriwa kuwa na muinuko wa kati ya mita 2500 kutoka usawa wa Bahari, hali hiyo inaifanya galigali kuwa na baridi kali.

02.3 MIUNDOMBINU
Miundombinu kama barabara haisadifu wala kufaa kwa usafiri, hakuna barabara halisi ya kufika huko na hata iliyopo ni ya mzunguko kutokea Mbuga ambayo nayo ni mbaya sana yenye tope, mashimo na haipitiki hasa kipindi cha masika, nyingne iliyopo hutokea chogora na kikuyu nayo ina mlima mrefu unaopelekea usafiri wa gali za kawaida kutokupanda isipokuwa aina ya “Land cruser na Defender” tu. Hata hivyo njia inapitika kwa pikipiki ambapo nauli yake ni elfu 20,000 kutoka Kikuyu hadi galigali.
Hakuna mawasiliano ya simu kwa urahisi kwa kuwa hakuna mtandao eneo lote linalokaliwa na watu kijijini hapo, hivyo mtu akitaka kuwasiliana kwa njia ya simu ni lazima apande mlimani umbali karibu wa Km 1 japo hutegemeana na eneo ulipo.

0.2.4 AFYA
Suala la afya kwa watu wa galigali ni tatizo kubwa, ipo zahanati ya kijiji lakini ifanyayo kazi kwa kusuasua. Ilitokea timu ya KGT ilipokuwa imefika huko, kutokana na safari ndefu, baadhi ya wanatimu walikuwa wakijisikia maumivu kiasi walichoona vema kutumia dawa za kutuliza maumivu (panardol), hata hivyo hazikupatikana kijiji kizima. Hali iliyotulazimu kuuliza watu wa eneo hilo wanaishije, wenyeji walijibu, “ndio hivyohivyo tunavyoishi” ikitokea kituo kiko wazi na dawa zipo tunapata huduma japo si sana, na wakaongeza kusema inaweza kupita wiki karibu tatu bila huduma kuwepo kwenye zahanati hiyo ya kijiji/selikali.

02.5 IMANI
Idadi kubwa ya wakazi wa galigali wanaoabudu ni waumini wa Roman Cathoric (RC), walio wengi hawaabudu na hawajui habari za wakovu hadi hapo Timu ilipowahubiria. Baadhi ya vitongoji vina waumini wa Anglikana ila kwa sababu ya kutokuwepo uamusho na mazingira mazuri ya ibada na mahali halisi pa kuabuddia imelifanya kanisa lisiwe na nguvu. Mfano galigali Yenyewe pamoja na kuwa na muhudumu (Shemashi) lakini bado hawana kanisa lolote kwa maana ya jengo hali inayowalazimu kutumia Dalasa la shule ya msingi galigali.
Watu wengi wa galigali wanaamini sana ushirikina, na miongoni mwao huamini kuwa ushirikina una nguvu kuliko hata Mungu, hivyo kinga yao ni kwa waganga wa kienyeji ambao ni wawili wanaoaminika.

KGT 
KGT ni kifupi cha Kuhani Gospel Team, kwa kiswahili  ni timu ya kikuhani ya Injili, inayohusika na kuwahubiri watu ili wamwamini Yesu Kristo na wampokea kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao, pia kuwafundisha ili wamjue Mungu wa pekee na kweli na Yesu Kristo aliyekuja duniani kwa ukombozi. Pia timu inahusika na kuwalea waliookoka, kuwaimarisha katika kumjua Kristo, kuwaandaa kuwa watumishi wenye kumtumikia Mungu kwa kiwango anachowakusudia, timu inagusa kila huduma ya Kiroho au iliyo katika ufalme wa Mungu hivyo kila mtu yaweza kumfaa maadamu ameokoka na anatamani kumtumikia Mungu. 
Timu hadi sasa ina Kanda Tatu, yaani Dodoma Mjini, Mpwapwa na Kongwa ambazo kwa pamoja hushirikiana miongoni mwa huduma na huduma nyingine kila kanda hujitegemea. Timu ina watumishi karibu 70, wanaotoka madhehebu tofauti, ikiwemo Romani Cathoric, EAGT, Anglikani, K.K.K.T, Moraviani, Kanisa la Mungu, TAG, FPCT, n.k, pia watumishi hawa hutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Timu inashirikiana na kanisa kwa ujumla wake, pia vikundi kama vile UKWATA, USCF, TYCS,TAFES, HUIMA,CASFETA,ASA kwa upande wa sekondari na vyuo, pia huduma mbalimbali kama vile Mana n.k, waimbaji binafsi na huduma za kijamii.
HUDUMA YA GALIGALI
Huduma hii ilifanywa na Timu ya KGT, kwa ushirika wa Kanisa kuu Anglikana ving’hawe ikiunganishwa na Rev. Capt. Canon, Anderson Madimilo. Wenyeji wa huduma hii walikuwa Kanisa Anglikana Galigali Dinari ya Kinusi, timu ilipata ushirika mkubwa kutoka kwa wenyeji ikiwa ni pamoja na chakula, malazi, maelekezo ya kihuduma, kibali selikali ya kijiji, n.k.
Timu ilifanya huduma ya uinjilist wa nyumba kwa nyumba mtaa kwa mtaa na shamba kwa shamba kwa muda wa siku nne (4) na mkutano siku sita (6). Katika huduma hiyo maeneo yaliyotembelewa na kufanyiwa huduma ni  Izumbawanu, Rugolovu, Mloa, Mfilo, Ngh’uluwe, Iwanginyi, Msingini, Mango, na galigali, nyumba zilizotembelewa na kufanyiwa huduma ni karibu 350, pia timu ilitembelea mashamba ya Kilimo kwa kuwa wakati huo ilikuwa msimu wa kilimo wengi wao walipatikana shambani kwa asubuhi na mchana.
Katika huduma hii watu 304 walimwamini na kumpokea Yesu Kristo kuwa BWANA na mwokozi wa maisha yao. 

YALIYOJILI WAKATI WA HUDUMA
Watu wa galigali katika masuala ya kiroho wako nyuma sana, na kufika kwa timu hii ya injili ilikuwa kama nuru na mwangaza mpya wa ujio wa ufalme wa Mungu kwa watu wa galigali. Timu ilistaajabu mazingira iliyoyakuta huko, hasa kutokana na uzoefu wa huduma ambazo timu ilikuwa imezifanya kabla kama Chamwino Ikulu na Mpwapwa ambapo kulikuwa na mwitikio mkubwa, mazingira yalikuwa tofauti timu ilipofika galigali.
Kwanza hakukuwa na eneo halisi la mkutano, pia hata timu ilipoanza kuhamasisha kwa kuimba nyimbo za kusifu hakukuwa na mwitikio wowote kutoka kwa wenyeji zaidi walitushangaa, hata timu iliposema Bwana Yesu asifiwe hawakuwa wanaelewa jinsi ya kupokea hivyo ilibidi timu Wenyewe wafanye jitihada za kuitika. 
Mazingira hayo yaliifanya timu ione na kuelewa maandiko yanayosema shambani mwa Bwana mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache, huwezi kuelewa maandiko hayo kama unaishi mjini au mahali ambapo kuna huduma za kiroho, pia timu ilimshukuru Mungu kwa kupata neeema hiyo maana sasa ilikuwa imeelewa utume na wito wa Yesu wakati anapaa, aliposema “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka na asiyeamini, atahukumiwa”.
Timu ililazimika kubadilisha mtazamo wa huduma na kuwa umisheni (mission), kwa kuwa isingetosha kufanya huduma ya kawaida.
Japo si kwa utafiti kamili, lakini inaonesha karibu asilimia 90 na zaidi ya  wenyeji wanakunywa pombe, timu ilipata shida sana, si nyumbani wala shambani, maana kila eneo watu walikutwa na pombe aidha wanakunywa au wanapika, kilichoshangaza ni pale timu ilipoenda shambani ili kuwafikia walioko huko na kuwahubiria, watu wale waliokuwa shambani nao walikuwa na pombe, ambayo walikunywa kama maji, hata wakati wa kuongea nao walitumia muda huo kunywa huku wakitusikiliza. wapo waliokubali kumpokea Yesu, lakini bado akiwa ameshika pombe, ilikuwa changamoto kubwa sana. Kiukweli wengi walimtaka Yesu lakini si kwa masharti ya kuacha pombe maana kwao ni utamaduni.
Jambo lililoshangaza zaidi, ni jinsi watu wale wanavyomwamini mganga wa kienyeji na kumheshimu kuliko mtu yeyote. Na hata kiongozi wa selikali kwao hana nguvu kuliko mganga wa kienyeji, hivyo baadhi ya kesi huamuliwa na mganga. Timu ilipowauliza waenyeji walisema hawawezi kuishi bila kupata msaada kutoka kwa waganga hao, na hivyo asilimia kubwa wana hilizi wanazozihesabu kama ulinzi, na tulipowaambaia habari za Mungu wa Kweli na wapekee, mwanzoni, baadhi walisema Mungu si zaidi ya mganga wa kijijini kwao.
Kutokana na hali hiyo timu iliamua kupanga safari ya kwenda kukutana na wanganga hao ili kuthibitisha kuwa Mungu wa Mbinguni anayeabudiwa katika Kristo Yesu ni zaidi ya kila kitu, wapo waliotusikitikia kwa kuona kuwa tutapata madhara endapo tutaonyesha kuwa kinyume na wanganga wao. Mmoja tulipokuwa tukienda alikimbia na tulipata nafasi ya kuonana na mmoja maana wako wawili waliosifika. Baada ya kuonana na huyo mmoja uso kwa uso alitetemeka kiasi cha sisi kumuonea huruma, ndipo tulipohojiana naye na akatueleza kila kitu anachokifanya na tulipomweleza habari za Kristo alikubaliana nazo na kusema yuko pamoja na sisi na sasa ataanza mabadiliko.
Hakukuwa na kanisa Anglikana zaidi liko kanisa la Roma, na waumini wachache sana wa dhehebu la Anglikana wanafanyia Ibada kwenye dalasa la shule ya msingi galigali. Na hawana Biblia wala tenzi wala standard wala mwongozo wowote wa ibada, baadhi ya wanatimu walilazimika kugawa vifaa vyao kwa wale walioonyesha kiu na walioipokea timu na kuihudumia vema. 

MSUKUMO WA TIMU KUTOKANA NA MAZINGIRA HAYO
Tmu ilpoona mazingira hayo haikusita kujadili ili kuona inaweza kufanya nini kwa hali hiyo, mapendekezo yaliyotolewa ilikuwa kama kuwasaidia baadhi ya wanafunzi wanaoonesha nia na kiu ya kuendelea, kwa mawazo ya baadhi ya wanatimu waliona kuwa hao wanaweza kuja kusaidia eneo hilo na kuwa na maendeleo ya kimwili na Kiroho. 
Hata hivyo jambo liliopata msukumo mkubwa na ambalo lilikuwa ndani ya timu ilikuwa suala la Afya. Timu ilipitisha adhima hiyo na iliwasilina na selikali ya kijiji na kufikisha adhima hiyo. Adhima ya timu ilikuwa ni angalau kufungua maabara ya vipimo kwa wagonjwa na duka la dawa muhimu/baridi. Lengo ikiwa ni kupunguza adha wanaoipata watu wa galigali katika suala la afya. Timu ilipolipeleka kwenye selikali ya kijiji liliungwa mkono kwa asilimia zote, na selikali ilitoa eneo la ujenzi wa maabara hiyo na duka.
Timu ilikuwa pia ikiwaza juu ya huduma za kiroho, lakini kwa kuwa timu haiwajibiki kujenga kanisa, ililiacha kama lilivyo ikaweka maadhimio ya kuwaombea, na kupata muda wa kurudi ili kuendeleza vuguvugu la wokovu.

UFUNUO NA MSUKUMO MPYA MIEZI 4 BAADA YA HUDUMA
Wakati timu ikiendelea kufanya maandalizi ya ujenzi wa maabara na duka, kwa kutafuta pesa za kuwezesha ujenzi na ufunguzi pamoja na kufuatilia taratibu za kibali kutoka selikalini, Roho Mtakatifu amekuwa akidokeza kuhusu maisha ya watu wale kiroho, lakini halikuwa linazingatiwa kwa kuwa kwa wajibu wa timu ulikuwa umekoma kwa huduma ile. 
Ilipofika mwezi wa kwanza (1) 2015, yalikuja maelekezo yaliyodokeza ujenzi wa Kanisa galigali, maelekezo hayo yalimshitua sana msimamizi wa timu na kumfanya ahoji kwa kumuomba Mungu nini maana yake na inawezekana vipi kujenga kanisa wakati timu siyo ya dhehebu flani wala hakuna maono ya kuwa dhehebu. Katikati ya kusumbuka, maelezo ya pili yalidokezwa, yaliyosema “inawapasa kusimamia ujenzi wa kanisa” bado huo ulikuwa mtihani mzito, lakini mfululizo huo wa pili ulieleza kuwa “Mimi Mungu siyatambui madhehebu kama ninyi mnavyoyaona, mimi nalitambua kanisa moja ambalo ni waamini na wanaoniabudu iwe ni kwa utaratibu wa kidhehebu au tofauti. 
Maelezo yaliendelea kudokeza kuwa, kwa kuwa kila kanisa kwa maana ya jengo ni lazima liwe kwa jina la dhehebu flan basi ninyi mtasimamia ujenzi wa kanisa la Kianglikana. Msimamizi alipopewa maelezo hayo, ilimuweka katika utata, maana Yeye mwenyewe alikuwa wa dhehebu la anglikana kiutaratibu, hivyo alijihoji na kuona kuwa jambo hilo linaweza kuleta matatizo katika timu, maana timu ina watu wa madhehebu tofauti, sasa ikiwa leo itaelezwa kuwa timu inasimamia ujenzi wa kanisa la kianglikana, ina maana kuwa yatatokea makundi na kuona kuwa timu inaanza kuwa ya kianglikana.
Ashukuriwe Mungu asiyefanya mambo kwa kubahatisha, alidokeza makusudi yake kwa kanisa kupitia timu, na hapo ilielezwa hivi; “Nimekusudia kuwapeleka maeneo yanayofanana na galigali mengi sana, ambayo yote yatawataka kuhubiri, kufundisha, kusaidia kuweka mazingira mazuri ya watu kuniamini na kuniabudu, kujenga makanisa na kuimarisha makusanyiko ya Ibada. Hata hivyo kila mahali nitakapowapeleka na kuwapa msukumo wa kufanya hivyo, basi ni wazi kuwa nitainua watu wa kanisa moja kuwaunga mkono, hivyo litajengwa kanisa litakalosimamiwa na kanisa hilo walioshiriki. Hivyo kwa galigali kwa ushirika wa Kanisa la Anglikana mtajenga kanisa la kianglikana na hao ndio niliowainua tangu mwanzo kwa ajili ya eneo hilo. 
07 MAELEKEZO YA KUKAMILISHI HAYO
Baada ya kulidhika na maelezo hayo, ilikuwa nikumuomba Mungu ili kujua pakuanzia na namna ya kulitekeleza, ndipo maelekezo yakatoka kuwa, kwa kuwa Eneo hilo liko Dayosisi ya Mpwapwa basi itawapasa kupata kibali kutoka huko, na kisha mtapata msaada kwa watu kutoa sadaka makanisani na nje ya Kanisa. Upatikanaji wa sadaka hizo utahusisha kanisa Anglikana moja kwa moja, timu watasimamia na kujitolea ili kuhakikisha jambo hili linatimia kwa mda na kwa uhakika.

MAOMBI, MAPENDEKEZO NA UFAFANUZI

 Timu inaomba Kanisa Anglikana, kutathimini juu ya huduma kama hii ya galigali na
 kuunga mkono timu hii Yenye nia ya kushirikiana na Kanisa kueneza na kuimalisha 
 Ufalme wa Mungu hapa Duniani.
 Timu inaomba Kanisa kuongeza nguvu katika kuendeleza utume na umisheni kwa 
 maeneo ambayo hali si nzuri katika huduma za Kiroho. 
 Timu inaomba Kanisa kutambua wito, karama, na vipawa vilivyoko katika kanisa na 
 kutumia hivyo katika kutimiza wajibu ambao kanisa lilipewa na Kristo
 Timu inaliomba Kanisa kushauri, kuelekeza, na kutoa utaratibu mwema wa kuisaidia timu  
 kutimiza wajibu wake wa kusaidiana na kanisa katika kutimiza agizo la Yesu Kristo la 
 kuhubiri, kufundisha, kulea, na kueneza ufalme wa Mungu.
 Timu inaliomba Kanisa kuisaidia Timu pale inapohitaji msaada wa uwezeshaji katika 
 kuandaa na kukamilisha huduma, msaada huo ni pamoja na kibali cha huduma, uenyeji  
 wa huduma, mawazo, vifaa, na mahitaji mengineyo, yote hayo kwa utaratibu maalumu na  
 wa kufaa.
 Ili kukamilisha huduma hii ya ujenzi wa kanisa huko galigali, timu iko radhi kushiriki 
 kwa kila namna inayofaa itakayokubaliwa na kanisa.

 Timu ilidokezwa kukusanya sadaka hizo kwa usihirika wa Kanisa na baada ya     
 kukamilika, Kanisa laweza kuwa na wawakilishi kadhaa na timu ikawa na wawakilishi   
 kadhaa ambao wataenda galilgali tayari kuanza ujenzi.
 Maeneo yanayopendekezwa na timu kukusanya/kutolewa sadaka ni mpwapwa, Kongwa, 
 Na Dodoma mjini. Timu ikishapata mapendekezo ya Kanisa na idhini ndipo itaanza   
 kushughulikia jambo hilo.
 Timu inadokeza kuwa, imesitisha baadhi ya huduma ili ijue hatima ya huduma hii, lengo 
 ni kuogopa kupanga huduma ambazo zinaweza kuliathiri hili, hivyo timu anaomba    
 kulitolea maamuzi mapema iwezekananyo ili kuisaidia timu kupanga mipango 
 isiyoathiliana.

MWISHO
Ashukuriwe Mungu Baba, Mungu Mwana tena Mungu Roho Mtakatifu, aliyetujalia neema ya kuwa watumishi wake katika shamba lake, Pia timu inalishukuru Kanisa Anglikana kwa ushirika wake Mkubwa, tena inayashukuru makanisa kama Anglikana kanisa kuu vingkhawe, St pauls, Kikuyu, na Kinusi, yote katika Dayosisi ya Mpwapwa kwa msaada wa kukamilisha huduma ya Galigali kwa sehemu na ni imani ya timu kuwa hapa palipobaki patamaiziwa kwa utukufu wa Mungu. Pia timu inawashukuru wachungaji wote wa makanisa hayo ikiwa ni pamoja na Rev. Capt. Canon Anderson Madimilo, Rev. capt. Agripa L.S. Ndatila, Rev Kingamkono  wote kwa ushirika wa kuisaidia timu zaidi kanda ya mpwapwa. 
Shukrani hizi ni  pamoja na kwa Rev. David Matonya Parishi ya chamwino, ambaye ni mshauri wa Timu Dodoma mjini.
Ni maombai ya timu juu ya Kanisa kuendelea mbele zaidi na kuimarika katika kila huduma inayofanya. 
Kwa niaba ya timu, KGT Dodoma mjini, Mpwapwa na Kongwa, niseme tunalipenda sana kanisa Angilikana Dodoma na Tanzania kwa ujumla.

Wako katika utumishi Goodluck Kazili, Msimamizi KGT-Tanzania

Mawasiliano
0765 129 960; Goodluck Kazili-Msimamizi KGT-Tanzania
0715 705 555; Mariamu Makasi- Msimamizi KGT- Mpwapwa
Email: kgteam11@yahoo.com au kgteam7@gmail.com 
Blog: kgtgoodluck.blogspot.com
www.facebook.com/KUHANI GOSPEL TEAM (KGT)

Jumatano, 11 Machi 2015

KUHANI GOSPEL TEAM (KGT) TAARIFA KUHUSU TIMU

KUHANI GOSPEL TEAM  

(KGT-TANZANIA)


TAARIFA KUHUSU TIMU

01. UTANGULIZI
KGT ni kifupi cha Kuhani Gospel Team kwa kiswahili Timu ya Kikuhani ya Injili, inayojihusisha na huduma za kuujenga ufalme wa Mungu/mbinguni hapa Duniani, huduma hizo ni pamoja na Mikutano ya Injili, uinjilisti wa nyumba kwa nyumba na maeneo ya mkusanyiko, uimbaji,Maombi na maombezi, Semina za Neno la Mungu, Malezi kwa waamini/waliookoka, Ushauri, kusaidia huduma, kusaidiana na kanisa kulinda na kuweka uchaji wa Mungu katika nchi

02. TIMU YENYEWE
Timu hii inaundwa na watu wanaoshuhudiwa kuwa wameitwa na kuteuliwa na Mungu kumtumikia Yeye, haina dhehebu wala Dini kwa maana ya kubagua ila ni timuya Kikristo kwa maaana ya inayomwamini na kumfuata Kristo Yesu. Inashirikiana na makanisa yote Yenye msingi wa Kristo, Inashirikiana na vikundi vyote vyenye msingi wa Kristo, inashirikiana na Watu wote wafanyao huduma katika msingi wa Kristo, na inajitoa kutumika mahali popote, mazingira yoyote na kwa namna yeyote maadamu kibali Cha Roho mtakatifu kipo.
Timu ina wahudumu zaidi ya 70, ambao wanaishi maeneo tofautitofauti katika nchi. Mfumo wa timu unamruhusu mtu kuwa katika timu akiwa popote ndani au nje ya nchi.
Timu imeweka watumishi walio washauri, ambao ni wachungaji wa makania tofautitofauti, watu wenye huduma mbalimbali wanaoshuhudiwa kuwa wema na wenye wito na mzigo na kazi ya Mungu, ambao kwa nafasi na neema ya Mungu iliyo juu yao, wanaijenga timu na kuifanya isonge mbele katika kutekeleza wajibu wa kuujenga ufalme wa Mungu, ili pia kufikia maono ya timu.

03. KUMBUKUMBU
Timu hii ilianza 11/2013, ikiwa na wanatimu karibu 30 waliounganishwa pamoja na Roho Mtakatifu na kuweka msukumo wa uundaji wa timu, miongoni mwa watu hao walikuwa wameshiriki huduma mbalimbali hasa wakiwa kama wanafunzi.
Mwezi huo wa 11 kwa usimamizi wa Roho Mtakatifu, Timu hii iliundwa rasmi kwa Ushirika wa Roho Mtakatifu, na sasa watu hawa waliweka maadhimio na mipango ya namna ya kuendelea mbele na mfumo utakaotumika ili kuifanya timu hii itimize wajibu ambao Roho mtakatifu anahimiza ndani yao.

2014 mwezi wa 6, Baada ya kufanya Huduma Katika wilaya ya Mpwapwa, Timu ilipata kibali cha kuunda timu katika wilaya ya Mpwapwa, timu hiyo iliundwa na kuwa kanda kamili ya KGT. Hivyo timu sasa iliendeshwa kikanda, kanda ya Dodoma mjini na kanda ya Mpwapwa.
Mwezi wa 9/2014 kwa mara ya kwanza kwa pamoja Timu kwa umoja na ushiriki wa Kanda zote ilifanya huduma Galigali kijiji kilichopo mpwapwa karibu na mkoa wa iringa, katika Huduma hiyo Dodoma mjini iliwakilishwa na wahudumu 13,  Mpwapwa iliwakilishwa na wahudumu 17. Katika huduma hiyo Timu ilishirikiana na Kanisa kuu Anglikana ving’hawe.
Mwezi wa 11/2014, Timu kwa kushirikiana na UKWATA Dodoma mjini, walifanya huduma Wilayani Kongwa, huduma ya mkutano na uinjilist wa nyumba kwa nyumba pamoja na Semina. Huduma hiyo iliyoratibiwa na umoja wa makanisa Kongwa ilifungua mlango wa Timu kuunda Kanda nyingine ya Kongwa. Hivyo kuifanya KGT kuwa na kanda Tatu.

04. MAONO YA KGT-TANZANIA
“Kumfanya kila mtu (katika mapenzi ya Mungu) amwamini, ampokee na kumjua Mungu wa pekee na kweli na Yesu Kristo aliyetumwa Duniani kwa ajili ya wokovu”

05. WAJIBU WA TIMU
Timu ina wajibu ambao ndio msingi wa kuundwa na kuwepo kwake, wajibu huo unagusa maeneo mawili:-

05.1. KWA MWANATIMU
“Kumsaidia kila mwanatimu kumtumikia Mungu kwa kiwango alichomkusudia”kwa maono haya, timu inawajibika kuangalia wito wa Mungu ndani ya kila mwanatimu na kumuandalia mazingira ya kutumika, ikiwa ni pamoja na kumwandaa ili kutumika sawasawa na mapenzi ya Mungu.

05.2. KWA WASIO WANATIMU
Kuwahubiri vema, ili wamwamini Yesu Kristo na kuupokea ufalme wa Mungu/mbinguni, kuwafundisha kumjua Mungu wa pekee na wa kweli na Yesu Kristo, kuwalea kwa Kusaidiana na Kanisa ili kutunza na kulinda wokovu walioupata ili wadumu katika Pendo la Mungu katika Ufalme wake.

06. KAULI MBIU
“Mjue Sana Mungu, Ili Uwe na Amani”

07. MSUKUMO NA MSIMAMO WA TIMU        KWA WANATIMU
“Kumuabudu Mungu, uzima hadi mauti, mauti hadi uzima, uzima na mauti hadi milele na milele”

08. KUTUMIKA KATIKA TIMU
Timu ina namna ya kutumika wakati wa huduma katika namna mbili, kuna utumishi wa kudumu na utumishi wa huduma.

08.1. UTUMISHI WA KUDUMU
Huu ni utumishi ambao mtumishi anakuwa sehemu halisi ya timu na anawajibika katika mambo yote yanayoihusu timu wakati wote, anahusika katika kupanga, kuamua na kujishughulisha na timu wakati wote, pia anajulishwa kila jambo na kuhusihswa katika uendeshwaji wa timu. Hadi sasa timu ina watumishi/wahudumu wa kudumu 70 kwa Kanda Zote.

08.2. UTUMISHI WA HUDUMA
Huu ni utumishi ambao mtumishi anashiriki huduma tu, ziko nyakati ambazo timu huwa na huduma sehemu mbalimbali katika mikoa, wilaya, vijiji na mitaa. Kwa mtumishi anayetambuliwa au aliyepata kibali cha kutumika kwa njia hii, wakati unapofika wa huduma Timu inampa taarifa na namna ya kushiriki katika huduma, na kisha mtumishi huyo huungana na timu tayari kwa kufanya huduma, baada ya huduma mtumishi hahusishwi na uendeleaji na uwajibikaji wa timu. Hadi sasa timu ina watumishi wa Huduma zaidi ya 10.

09. MFUMO WA KGT
Timu ina mfamo wa uendeshaji unaoisaidia timu kuendelea mbele na kutimiza wajibu iliopewa na Mungu. Timu ina mfumo wa Kanda kimaeneo na zote hutumia mfumo mmoja katika uendeshaji wa timu ngazi ya kanda. Pia ina mfumo wa idara za utendaji kazi/huduma kulingana na karama na vipawa vya kutumika. Timu ina idara 6 zinazosimamia shughuli zote katika timu. Katika idala yuko/wako wasimamizi wa Idala hizo na waliosalia wote ni wajumbe wa Idala kulingana na Karama pamoja na kipawa alichonacho. Timu inajumuisha watu wa lika zote, katika kusimamia, suala la lika halihusiki sana, zaidi ni uwezo na jinsi karama inavyofanya kazi ndani ya mtu.

10. IDARA ZA KGT
10.1. KGT UTATU
Hii ni Idara ambayo ndani yake limo kundi la uombaji, uinjilist, malezi, ushauri na maelekezi. Idara hii huratibu shughuli zote na kuwajibika ipasavyo ili kutimiza mambo yanayoangukia kwenye idara hiyo kwa kila kudi kama yalivyo. Mfumo huu wa kiutendaji ni wa kanda zote, hata hiyvo Idara ina wasimamizi watatu kwa kila kanda na ni wazi kuwa timu ikiongezeka basi wasimamizi hao huongezwa.

10.2. KGT HAZINA
Hii ni idara inayosimamia Sadaka na upatikanaji wa mahitaji mbalimbali katika timu ili huduma zisikwame kwa uhitajiwa wa fedha na vitu. Idara hii inahusika na kuomba, kujua na kutekeleza upatikanaji wa mahitaji mbalimbali ya kuisaidia timu kuendesha huduma, pia idara inahusika na kuhifadhi, kutunza na kulinda ili timu iwe na hazina ya kutosha.

10.3. KGT HABARI NA MAWASILIANO
Hii ni idara inayoratibu masuala yote ya kutoa na kupokea habari/taarifa kutoka na kwenda mahali husika. Pia inahusika katika kufungua na kusimamia vyombo vinavyohusika na utoajia habari kama vile mitandao ya kijamii, redio, runinga na simu.
Idara hii inashirikiana na idara ya “KGT production”katika kuandaa matangazo, kuzalisha na kusambaza kazi za huduma ili kutimiza wajibu wa timu wa kuwafikia wengi kwa njia za kila namna.

10.4. KGT PRODUCTION
Idara hii inahusika na kuandaa matangazo, kuchukua kumbukumbu za huduma, kusambaza kazi za huduma kama vile tape, CD, DVD na machapisho. Pia Idara hii hushirikiana na idara maalumu kuweka mazingra mazri ya huduma.

10.5. KGT WORSHIP
Idara hii, inahusika na masuala yote ya uimbaji wakati wa huduma za timu na wakati mwingine wowote inapopaswa kuhudumu. Pia idara hii, inahusika kuibua, kuchochoe na kusimamia watu wenye wito wa kuimba wafanye vema katika wito huo, ikiwa ni pamoja na kuwaandaa na kuwaatengenezea mazingra ya kutumika kwa kiwango stahiki.

10.6. IDARA MAALUMU
Hii ni idara inayohusika na kuratibu shughuli zote zisizoangukia katika idala zilizotajwa, shughuli hizo ni pamoja na masuala ya kusaidiana, masuala ya chakula wakati wa huduma, kusimamia Muonekano wa wanatimu Hasa wakati wa huduma, kubuni vitu vinavyoendeleza timu kwa mtazamo wa kiroho na kimwili.

11. HUDUMA KATIKA TIMU
Timu hii kwa mujibu wa ufunuo wa kuundwa kwake na maono ya uendeshwaji wake, timu inajikita katika kufanya huduma zaidi na kuwaandaa watumishi. Hivyo huduma zilizo kuu ni kuwatangazia watu habari za ufalme wa Mungu, kwa njia ya kuwahubiri na kuwaombea, pia kuwafundisha ili wajue jinsi ufalme wa Mungu ulivyo kwa njia ya Semina. Kufanya ibada kama timu ikiwa ni kuendelea kuleana na kuimarika ili kuwa na uwezo wa kufanya huduma sawasawa na mapenzi ya Mungu.
Timu inajikita maeneo ya miji midogo na vijiji hasa maeneo ambayo Injili haijawafikia Vema. Katika hayo timu inafanya mikutano ya injili, na hupeleka semina kila mwaka katika maeneo yote iliyokwisha fanya huduma ya uinjilist nia ikiwa ni kuzaa matunda na kulea na syo kuzaa tu.
Ziko huduma zifanywazo na kanda, lakini pia zipo huduma za ngazi ya timu. Huduma za kanda zinafanyika katika eneo linaloizunguka kanda kwa upana wake, na huduma za ngazi ya timu zinafanyika eneo lolote.

12. MWISHO
Timu hii, ina nia ya kutumika kwelikweli kwa kadri neema ya Mungu inavyofunuliwa. Inalenga kupanuka kuimarika na kukua zaidi. Inaendelea kuomba ili kujua mapenzi ya Mungu kamili katika nchi na watu, kuendelea kuweka mfumo wa kutumika zaidi na kufikia ukomo mwema wa uimalikaji wa kila mtu katika ufalme wa Mungu. Timu inaendelea kusimama vema, kuhakikisha inatimiza wito huo kwa gharama yoyote, kwa maana hiyo, timu hailegei wala haichoki katika hali yoyote, katika mazingira yote ina imarika na itaimarika zaidi na zaidi. “KGT-TANZANIA, Mjue Sana Mungu Ili uwe na Amani”

Kunihusu

Picha yangu
"Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, baba , kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. (Ni Siri Kuu)

Tafuta katika Blogu Hii