01. UTANGULIZI
Hii ni Taarifa ya KUHANI GOSPEL TEAM (KGT) juu ya huduma ya kiroho iliyofanyika Galigali, huduma ilifanyika tarehe 7/09 hadi 14/09/2014. Katika huduma hii timu ya watu 30 walishiriki, 17 wakitokea Mpwapwa na 13 wakitokea Dodoma mjini. Huduma kubwa iliyofanyika ni ya uinjilist wa kitongoji kwa kitongoji, shamba kwa shamba, nyumba kwa nyumba pamoja na mkutano.
02 GALIGALI YENYEWE
02.1 KIUTAWALA/KISELIKALI
Galigali inaundwa na maeneo/vitongoji karibu 7 ikiwemo Izumbawanu, Mlowa, Mfilo, Iwanginyi, Ngh’uluwe, Dibulilo na kakwandali. Inakadiliwa kuwa na wakazi zaidi ya 3000 na kaya zaidi ya 600.
02.2 KIJOGORAFIA
kijogorafia galigali iko mlimani, kuna umbali wa Km 20 kutoka mbuga, imezungukwa na vijiji kama mbuga, lufu, makosa, makoleko, chogora, kikuyu na matonya. Ina vitongoji 7 na imezungukwa na milima mikubwa inayofanya miundombinu ya Barabara na mawasiliano kuwa magumu. Hali ya hewa ni nzuri kwa kilimo, imezungukwa na misitu na milima inayofanya nvua kuwa nyingi, inakadriwa kuwa na muinuko wa kati ya mita 2500 kutoka usawa wa Bahari, hali hiyo inaifanya galigali kuwa na baridi kali.
02.3 MIUNDOMBINU
Miundombinu kama barabara haisadifu wala kufaa kwa usafiri, hakuna barabara halisi ya kufika huko na hata iliyopo ni ya mzunguko kutokea Mbuga ambayo nayo ni mbaya sana yenye tope, mashimo na haipitiki hasa kipindi cha masika, nyingne iliyopo hutokea chogora na kikuyu nayo ina mlima mrefu unaopelekea usafiri wa gali za kawaida kutokupanda isipokuwa aina ya “Land cruser na Defender” tu. Hata hivyo njia inapitika kwa pikipiki ambapo nauli yake ni elfu 20,000 kutoka Kikuyu hadi galigali.
Hakuna mawasiliano ya simu kwa urahisi kwa kuwa hakuna mtandao eneo lote linalokaliwa na watu kijijini hapo, hivyo mtu akitaka kuwasiliana kwa njia ya simu ni lazima apande mlimani umbali karibu wa Km 1 japo hutegemeana na eneo ulipo.
0.2.4 AFYA
Suala la afya kwa watu wa galigali ni tatizo kubwa, ipo zahanati ya kijiji lakini ifanyayo kazi kwa kusuasua. Ilitokea timu ya KGT ilipokuwa imefika huko, kutokana na safari ndefu, baadhi ya wanatimu walikuwa wakijisikia maumivu kiasi walichoona vema kutumia dawa za kutuliza maumivu (panardol), hata hivyo hazikupatikana kijiji kizima. Hali iliyotulazimu kuuliza watu wa eneo hilo wanaishije, wenyeji walijibu, “ndio hivyohivyo tunavyoishi” ikitokea kituo kiko wazi na dawa zipo tunapata huduma japo si sana, na wakaongeza kusema inaweza kupita wiki karibu tatu bila huduma kuwepo kwenye zahanati hiyo ya kijiji/selikali.
02.5 IMANI
Idadi kubwa ya wakazi wa galigali wanaoabudu ni waumini wa Roman Cathoric (RC), walio wengi hawaabudu na hawajui habari za wakovu hadi hapo Timu ilipowahubiria. Baadhi ya vitongoji vina waumini wa Anglikana ila kwa sababu ya kutokuwepo uamusho na mazingira mazuri ya ibada na mahali halisi pa kuabuddia imelifanya kanisa lisiwe na nguvu. Mfano galigali Yenyewe pamoja na kuwa na muhudumu (Shemashi) lakini bado hawana kanisa lolote kwa maana ya jengo hali inayowalazimu kutumia Dalasa la shule ya msingi galigali.
Watu wengi wa galigali wanaamini sana ushirikina, na miongoni mwao huamini kuwa ushirikina una nguvu kuliko hata Mungu, hivyo kinga yao ni kwa waganga wa kienyeji ambao ni wawili wanaoaminika.
KGT
KGT ni kifupi cha Kuhani Gospel Team, kwa kiswahili ni timu ya kikuhani ya Injili, inayohusika na kuwahubiri watu ili wamwamini Yesu Kristo na wampokea kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao, pia kuwafundisha ili wamjue Mungu wa pekee na kweli na Yesu Kristo aliyekuja duniani kwa ukombozi. Pia timu inahusika na kuwalea waliookoka, kuwaimarisha katika kumjua Kristo, kuwaandaa kuwa watumishi wenye kumtumikia Mungu kwa kiwango anachowakusudia, timu inagusa kila huduma ya Kiroho au iliyo katika ufalme wa Mungu hivyo kila mtu yaweza kumfaa maadamu ameokoka na anatamani kumtumikia Mungu.
Timu hadi sasa ina Kanda Tatu, yaani Dodoma Mjini, Mpwapwa na Kongwa ambazo kwa pamoja hushirikiana miongoni mwa huduma na huduma nyingine kila kanda hujitegemea. Timu ina watumishi karibu 70, wanaotoka madhehebu tofauti, ikiwemo Romani Cathoric, EAGT, Anglikani, K.K.K.T, Moraviani, Kanisa la Mungu, TAG, FPCT, n.k, pia watumishi hawa hutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Timu inashirikiana na kanisa kwa ujumla wake, pia vikundi kama vile UKWATA, USCF, TYCS,TAFES, HUIMA,CASFETA,ASA kwa upande wa sekondari na vyuo, pia huduma mbalimbali kama vile Mana n.k, waimbaji binafsi na huduma za kijamii.
HUDUMA YA GALIGALI
Huduma hii ilifanywa na Timu ya KGT, kwa ushirika wa Kanisa kuu Anglikana ving’hawe ikiunganishwa na Rev. Capt. Canon, Anderson Madimilo. Wenyeji wa huduma hii walikuwa Kanisa Anglikana Galigali Dinari ya Kinusi, timu ilipata ushirika mkubwa kutoka kwa wenyeji ikiwa ni pamoja na chakula, malazi, maelekezo ya kihuduma, kibali selikali ya kijiji, n.k.
Timu ilifanya huduma ya uinjilist wa nyumba kwa nyumba mtaa kwa mtaa na shamba kwa shamba kwa muda wa siku nne (4) na mkutano siku sita (6). Katika huduma hiyo maeneo yaliyotembelewa na kufanyiwa huduma ni Izumbawanu, Rugolovu, Mloa, Mfilo, Ngh’uluwe, Iwanginyi, Msingini, Mango, na galigali, nyumba zilizotembelewa na kufanyiwa huduma ni karibu 350, pia timu ilitembelea mashamba ya Kilimo kwa kuwa wakati huo ilikuwa msimu wa kilimo wengi wao walipatikana shambani kwa asubuhi na mchana.
Katika huduma hii watu 304 walimwamini na kumpokea Yesu Kristo kuwa BWANA na mwokozi wa maisha yao.
YALIYOJILI WAKATI WA HUDUMA
Watu wa galigali katika masuala ya kiroho wako nyuma sana, na kufika kwa timu hii ya injili ilikuwa kama nuru na mwangaza mpya wa ujio wa ufalme wa Mungu kwa watu wa galigali. Timu ilistaajabu mazingira iliyoyakuta huko, hasa kutokana na uzoefu wa huduma ambazo timu ilikuwa imezifanya kabla kama Chamwino Ikulu na Mpwapwa ambapo kulikuwa na mwitikio mkubwa, mazingira yalikuwa tofauti timu ilipofika galigali.
Kwanza hakukuwa na eneo halisi la mkutano, pia hata timu ilipoanza kuhamasisha kwa kuimba nyimbo za kusifu hakukuwa na mwitikio wowote kutoka kwa wenyeji zaidi walitushangaa, hata timu iliposema Bwana Yesu asifiwe hawakuwa wanaelewa jinsi ya kupokea hivyo ilibidi timu Wenyewe wafanye jitihada za kuitika.
Mazingira hayo yaliifanya timu ione na kuelewa maandiko yanayosema shambani mwa Bwana mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache, huwezi kuelewa maandiko hayo kama unaishi mjini au mahali ambapo kuna huduma za kiroho, pia timu ilimshukuru Mungu kwa kupata neeema hiyo maana sasa ilikuwa imeelewa utume na wito wa Yesu wakati anapaa, aliposema “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka na asiyeamini, atahukumiwa”.
Timu ililazimika kubadilisha mtazamo wa huduma na kuwa umisheni (mission), kwa kuwa isingetosha kufanya huduma ya kawaida.
Japo si kwa utafiti kamili, lakini inaonesha karibu asilimia 90 na zaidi ya wenyeji wanakunywa pombe, timu ilipata shida sana, si nyumbani wala shambani, maana kila eneo watu walikutwa na pombe aidha wanakunywa au wanapika, kilichoshangaza ni pale timu ilipoenda shambani ili kuwafikia walioko huko na kuwahubiria, watu wale waliokuwa shambani nao walikuwa na pombe, ambayo walikunywa kama maji, hata wakati wa kuongea nao walitumia muda huo kunywa huku wakitusikiliza. wapo waliokubali kumpokea Yesu, lakini bado akiwa ameshika pombe, ilikuwa changamoto kubwa sana. Kiukweli wengi walimtaka Yesu lakini si kwa masharti ya kuacha pombe maana kwao ni utamaduni.
Jambo lililoshangaza zaidi, ni jinsi watu wale wanavyomwamini mganga wa kienyeji na kumheshimu kuliko mtu yeyote. Na hata kiongozi wa selikali kwao hana nguvu kuliko mganga wa kienyeji, hivyo baadhi ya kesi huamuliwa na mganga. Timu ilipowauliza waenyeji walisema hawawezi kuishi bila kupata msaada kutoka kwa waganga hao, na hivyo asilimia kubwa wana hilizi wanazozihesabu kama ulinzi, na tulipowaambaia habari za Mungu wa Kweli na wapekee, mwanzoni, baadhi walisema Mungu si zaidi ya mganga wa kijijini kwao.
Kutokana na hali hiyo timu iliamua kupanga safari ya kwenda kukutana na wanganga hao ili kuthibitisha kuwa Mungu wa Mbinguni anayeabudiwa katika Kristo Yesu ni zaidi ya kila kitu, wapo waliotusikitikia kwa kuona kuwa tutapata madhara endapo tutaonyesha kuwa kinyume na wanganga wao. Mmoja tulipokuwa tukienda alikimbia na tulipata nafasi ya kuonana na mmoja maana wako wawili waliosifika. Baada ya kuonana na huyo mmoja uso kwa uso alitetemeka kiasi cha sisi kumuonea huruma, ndipo tulipohojiana naye na akatueleza kila kitu anachokifanya na tulipomweleza habari za Kristo alikubaliana nazo na kusema yuko pamoja na sisi na sasa ataanza mabadiliko.
Hakukuwa na kanisa Anglikana zaidi liko kanisa la Roma, na waumini wachache sana wa dhehebu la Anglikana wanafanyia Ibada kwenye dalasa la shule ya msingi galigali. Na hawana Biblia wala tenzi wala standard wala mwongozo wowote wa ibada, baadhi ya wanatimu walilazimika kugawa vifaa vyao kwa wale walioonyesha kiu na walioipokea timu na kuihudumia vema.
MSUKUMO WA TIMU KUTOKANA NA MAZINGIRA HAYO
Tmu ilpoona mazingira hayo haikusita kujadili ili kuona inaweza kufanya nini kwa hali hiyo, mapendekezo yaliyotolewa ilikuwa kama kuwasaidia baadhi ya wanafunzi wanaoonesha nia na kiu ya kuendelea, kwa mawazo ya baadhi ya wanatimu waliona kuwa hao wanaweza kuja kusaidia eneo hilo na kuwa na maendeleo ya kimwili na Kiroho.
Hata hivyo jambo liliopata msukumo mkubwa na ambalo lilikuwa ndani ya timu ilikuwa suala la Afya. Timu ilipitisha adhima hiyo na iliwasilina na selikali ya kijiji na kufikisha adhima hiyo. Adhima ya timu ilikuwa ni angalau kufungua maabara ya vipimo kwa wagonjwa na duka la dawa muhimu/baridi. Lengo ikiwa ni kupunguza adha wanaoipata watu wa galigali katika suala la afya. Timu ilipolipeleka kwenye selikali ya kijiji liliungwa mkono kwa asilimia zote, na selikali ilitoa eneo la ujenzi wa maabara hiyo na duka.
Timu ilikuwa pia ikiwaza juu ya huduma za kiroho, lakini kwa kuwa timu haiwajibiki kujenga kanisa, ililiacha kama lilivyo ikaweka maadhimio ya kuwaombea, na kupata muda wa kurudi ili kuendeleza vuguvugu la wokovu.
UFUNUO NA MSUKUMO MPYA MIEZI 4 BAADA YA HUDUMA
Wakati timu ikiendelea kufanya maandalizi ya ujenzi wa maabara na duka, kwa kutafuta pesa za kuwezesha ujenzi na ufunguzi pamoja na kufuatilia taratibu za kibali kutoka selikalini, Roho Mtakatifu amekuwa akidokeza kuhusu maisha ya watu wale kiroho, lakini halikuwa linazingatiwa kwa kuwa kwa wajibu wa timu ulikuwa umekoma kwa huduma ile.
Ilipofika mwezi wa kwanza (1) 2015, yalikuja maelekezo yaliyodokeza ujenzi wa Kanisa galigali, maelekezo hayo yalimshitua sana msimamizi wa timu na kumfanya ahoji kwa kumuomba Mungu nini maana yake na inawezekana vipi kujenga kanisa wakati timu siyo ya dhehebu flani wala hakuna maono ya kuwa dhehebu. Katikati ya kusumbuka, maelezo ya pili yalidokezwa, yaliyosema “inawapasa kusimamia ujenzi wa kanisa” bado huo ulikuwa mtihani mzito, lakini mfululizo huo wa pili ulieleza kuwa “Mimi Mungu siyatambui madhehebu kama ninyi mnavyoyaona, mimi nalitambua kanisa moja ambalo ni waamini na wanaoniabudu iwe ni kwa utaratibu wa kidhehebu au tofauti.
Maelezo yaliendelea kudokeza kuwa, kwa kuwa kila kanisa kwa maana ya jengo ni lazima liwe kwa jina la dhehebu flan basi ninyi mtasimamia ujenzi wa kanisa la Kianglikana. Msimamizi alipopewa maelezo hayo, ilimuweka katika utata, maana Yeye mwenyewe alikuwa wa dhehebu la anglikana kiutaratibu, hivyo alijihoji na kuona kuwa jambo hilo linaweza kuleta matatizo katika timu, maana timu ina watu wa madhehebu tofauti, sasa ikiwa leo itaelezwa kuwa timu inasimamia ujenzi wa kanisa la kianglikana, ina maana kuwa yatatokea makundi na kuona kuwa timu inaanza kuwa ya kianglikana.
Ashukuriwe Mungu asiyefanya mambo kwa kubahatisha, alidokeza makusudi yake kwa kanisa kupitia timu, na hapo ilielezwa hivi; “Nimekusudia kuwapeleka maeneo yanayofanana na galigali mengi sana, ambayo yote yatawataka kuhubiri, kufundisha, kusaidia kuweka mazingira mazuri ya watu kuniamini na kuniabudu, kujenga makanisa na kuimarisha makusanyiko ya Ibada. Hata hivyo kila mahali nitakapowapeleka na kuwapa msukumo wa kufanya hivyo, basi ni wazi kuwa nitainua watu wa kanisa moja kuwaunga mkono, hivyo litajengwa kanisa litakalosimamiwa na kanisa hilo walioshiriki. Hivyo kwa galigali kwa ushirika wa Kanisa la Anglikana mtajenga kanisa la kianglikana na hao ndio niliowainua tangu mwanzo kwa ajili ya eneo hilo.
07 MAELEKEZO YA KUKAMILISHI HAYO
Baada ya kulidhika na maelezo hayo, ilikuwa nikumuomba Mungu ili kujua pakuanzia na namna ya kulitekeleza, ndipo maelekezo yakatoka kuwa, kwa kuwa Eneo hilo liko Dayosisi ya Mpwapwa basi itawapasa kupata kibali kutoka huko, na kisha mtapata msaada kwa watu kutoa sadaka makanisani na nje ya Kanisa. Upatikanaji wa sadaka hizo utahusisha kanisa Anglikana moja kwa moja, timu watasimamia na kujitolea ili kuhakikisha jambo hili linatimia kwa mda na kwa uhakika.
MAOMBI, MAPENDEKEZO NA UFAFANUZI
Timu inaomba Kanisa Anglikana, kutathimini juu ya huduma kama hii ya galigali na
kuunga mkono timu hii Yenye nia ya kushirikiana na Kanisa kueneza na kuimalisha
Ufalme wa Mungu hapa Duniani.
Timu inaomba Kanisa kuongeza nguvu katika kuendeleza utume na umisheni kwa
maeneo ambayo hali si nzuri katika huduma za Kiroho.
Timu inaomba Kanisa kutambua wito, karama, na vipawa vilivyoko katika kanisa na
kutumia hivyo katika kutimiza wajibu ambao kanisa lilipewa na Kristo
Timu inaliomba Kanisa kushauri, kuelekeza, na kutoa utaratibu mwema wa kuisaidia timu
kutimiza wajibu wake wa kusaidiana na kanisa katika kutimiza agizo la Yesu Kristo la
kuhubiri, kufundisha, kulea, na kueneza ufalme wa Mungu.
Timu inaliomba Kanisa kuisaidia Timu pale inapohitaji msaada wa uwezeshaji katika
kuandaa na kukamilisha huduma, msaada huo ni pamoja na kibali cha huduma, uenyeji
wa huduma, mawazo, vifaa, na mahitaji mengineyo, yote hayo kwa utaratibu maalumu na
wa kufaa.
Ili kukamilisha huduma hii ya ujenzi wa kanisa huko galigali, timu iko radhi kushiriki
kwa kila namna inayofaa itakayokubaliwa na kanisa.
Timu ilidokezwa kukusanya sadaka hizo kwa usihirika wa Kanisa na baada ya
kukamilika, Kanisa laweza kuwa na wawakilishi kadhaa na timu ikawa na wawakilishi
kadhaa ambao wataenda galilgali tayari kuanza ujenzi.
Maeneo yanayopendekezwa na timu kukusanya/kutolewa sadaka ni mpwapwa, Kongwa,
Na Dodoma mjini. Timu ikishapata mapendekezo ya Kanisa na idhini ndipo itaanza
kushughulikia jambo hilo.
Timu inadokeza kuwa, imesitisha baadhi ya huduma ili ijue hatima ya huduma hii, lengo
ni kuogopa kupanga huduma ambazo zinaweza kuliathiri hili, hivyo timu anaomba
kulitolea maamuzi mapema iwezekananyo ili kuisaidia timu kupanga mipango
isiyoathiliana.
MWISHO
Ashukuriwe Mungu Baba, Mungu Mwana tena Mungu Roho Mtakatifu, aliyetujalia neema ya kuwa watumishi wake katika shamba lake, Pia timu inalishukuru Kanisa Anglikana kwa ushirika wake Mkubwa, tena inayashukuru makanisa kama Anglikana kanisa kuu vingkhawe, St pauls, Kikuyu, na Kinusi, yote katika Dayosisi ya Mpwapwa kwa msaada wa kukamilisha huduma ya Galigali kwa sehemu na ni imani ya timu kuwa hapa palipobaki patamaiziwa kwa utukufu wa Mungu. Pia timu inawashukuru wachungaji wote wa makanisa hayo ikiwa ni pamoja na Rev. Capt. Canon Anderson Madimilo, Rev. capt. Agripa L.S. Ndatila, Rev Kingamkono wote kwa ushirika wa kuisaidia timu zaidi kanda ya mpwapwa.
Shukrani hizi ni pamoja na kwa Rev. David Matonya Parishi ya chamwino, ambaye ni mshauri wa Timu Dodoma mjini.
Ni maombai ya timu juu ya Kanisa kuendelea mbele zaidi na kuimarika katika kila huduma inayofanya.
Kwa niaba ya timu, KGT Dodoma mjini, Mpwapwa na Kongwa, niseme tunalipenda sana kanisa Angilikana Dodoma na Tanzania kwa ujumla.
Wako katika utumishi Goodluck Kazili, Msimamizi KGT-Tanzania
Mawasiliano
0765 129 960; Goodluck Kazili-Msimamizi KGT-Tanzania
0715 705 555; Mariamu Makasi- Msimamizi KGT- Mpwapwa
Email: kgteam11@yahoo.com au kgteam7@gmail.com
Blog: kgtgoodluck.blogspot.com
www.facebook.com/KUHANI GOSPEL TEAM (KGT)