KUHANI GOSPEL TEAM (KGT)TANZANIA)
SIRAHA MHIMU ZA UFALME WA MUNGU
Linapotajwa
Neno siraha, kuna kitu kinajengeka ndani yako, na wakati mwingine utapata picha
fulani. Hata hivyo suala la siraha lipo ikiwa tu kuna vita au ulinzi au
uharibifu. Kama ilivyo katika mwili pia katika
ulimwengu wa roho zipo siraha, na
zinamatumizi mbalimbali.
Mpendwa
katika Kristo, ni wazi kuwa, siraha hizi za ufalme wa Mungu, ni mhimu kuzijua
zote pamoja na matumizi yake, lakini pia umhimu wake.
Waefeso
6:10, inaeleza kuwa tuzidi kuwa hodari katika uweza wa Mungu na nguvu zake,
lakini anasema uhodari wetu upo kwa kuzivaa siraha zote za MUNGU. Hapa
unagundua kuwa zipo siraha nyingi za MUNGU, na ikiwa zipo nyingi zaidi ya moja kama maandiko yanavyothibitisha, basi ni hakika kuwa,
zinatofautiana katika matumizi pia.
MUNGU
alipotengeneza siraha tofauti tofauti, alikuwa na maana kubwa, na siraha hizo
hutumika kwa wanadamu tu na zipo zitumikazo kwa malaika, ila hatutazungumzia
hizo za malaika ila tutazungumzia zilizowekwa kutumiwa na wanadamu au duniani. Kama nilivyoeleza kuwa siraha hizo zinatofautiana kwa
namna nyingi.
Mtumiaji wa
siraha
Huyu
ni mtu mhimu sana kwa kuwa siraha za Mungu zilizotengenezwa kwa ajili ya wana
wa ufalme wa MUNGU hapa duniani, haziwezi fanya kazi hadi awepo mtumiaji, na
kama mtumiaji atakosa maarifa basi siraha hizo zitafanya kazi kwa kiwango cha
maarifa alichonacho mtumiaji.
AINA ZA
SIRAHA ZA UFALME WA MUNGU
SIRAHA YA IMANI
Hii
ni siraha ya kwanza, si kwa ukubwa ila inayobeba siraha nyingine pia. Kwa mjibu
wa waebrania 11:1 imani ni kuwa na hakika), si kitu cha kubahatisha, ila ni
uhakika ambao mtu anakuwa nao juu ya jambo Fulani, tena jambo hilo lisiwe la wakati huo ila liwe la wakati
ujao na lazima liwe halionekani. Ukisikia kitu kisichoonekana ina maana kuwa
kitu hicho ni cha kiroho.
Kwa
maana nyingine tunaweza kusema, imani ni namna ya roho inayosimama kama nguvu, siraha, mamlaka, uwezo, uhakika na kuamini,
inayotarajia kutekeleza au kutekelezwa kwa jambo fulani. Kwa msingi huo imani
si kuamini tu kuwa Mungu anaweza ila ni zaidi ya kumwamini MUNGU. Mwili una kawaida ya kutokuamini vitu vya
rohoni, hivyo wakati mwingine mwili unaweza kukutia moyo kuwa Mungu anaweza
kila kitu ila ikifika kwenye tatizo mwili utakuambia hili siyo la kawaida.
Lengo la kukuambia hivyo ni ili kukuondoa kwenye imani halisi ya utendaji
ambayo ndiyo kubwa.
Kuna
imani ya kumwamini Mungu kuwa anaweza, lakini pia kuna imani zaidi ya kumwamini
Mungu kuwa anaweza. Ukweli ni kuwa kitendo cha kumwamini Mungu kuwa anaweza ni
hatua ya kwanza ya imani, kuishia hapo hakuwezi kusaidia kitu zaidi ya kuwa na
tumaini tu, lakini ukitaka kuiona, imani ikifanya kazi yake, lazima kuamini
huko ukufanye kuwa kitendo.
Mfano
mama hana mtoto, na ameomba na kuhitaji sana kupata mtoto na hajapata, kwa hakika
ni kuwa mama huyo anaweza akawa anamwamini Mungu lakini kumwamini Mungu huko
hakuwezi kumsaidia asilimia nyingi kupata mtoto, isipokuwa kinachoweza
kumsaidia ni pale anapoweza kubadili ile hali ya kuamini, iwe tendo.
Mfano
mama anaweza kuamua na kusema, kwa kuwa imani ni kuwa na hakika ya mambo
yatarajiwayo na ni yale mambo yasiyoonekana, hivyo basi itampasa kuwa na
uhakika ndani kuwa, mwakani atakuwa na mtoto na inampasa kufanya
maandalizi kwa kuanza kununua vifaa
vyote vya mtoto atakayemzaa, na wakati huo pengine hata mimbabado. Mungu akiiona imani hiyo hakika lazima
amfanyie mama huyo hata kama mpango haukuwepo.
Ukisoma
maandiko matakatifu, unagundua kuwa wakati Yesu alipokuwa akiendelea na huduma
kati ya vitu alivyokuwa anaangalia ilikuwa imani ya mtu, wakati mwingine hata kama mtu alikuwa hasitahili kutendewa lakini kwa imani
yake ilimulazimu Yesu kumfanyia haja yake.
Nakuomba
usome kwa umakini mistari hii uione imani jinsi ilivyo na hapa ndipo Roho
alipokusudia kukufundishia suala la imani
“(Mathayo
15:22-28), Natazama, mwanamke mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia
sauti akisema, unirehemu, Bwana, mwana wa Daud; binti yangu amepagawa sana na mapepo. 23 Wala Yeye hakumjibu neno. nao wanafunzi
wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema
mwache aende zake; maana anapiga kelele nyuma yetu. 24 Akajibu, akasema, sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. 25 Naye akaja akamsujudia, akasema Bwana, unisaidie.
26 Akajibu, akasema, si vema kukitwaa
chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. 27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa
hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. 28 Ndipo Yesu akajibu,
akamwambia, mama imani yako ni kubwa; na
iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti
yake tangu saa ile”
Sijui
umepata kitu gani, lakini kwa kweli huwezi kuielewa imani vema hadi umeyapima
mazingira na mazungumzo ya huyu mama na Yesu. Maneno yaliyolazwa ni kauli za
mama mkananyo, maneno yaliyokolezwa na hayajalazwa ni ya Yesu mwenyewe na
mengine walisema wanafunzi.
Kama
umefuatilia kwa nia ya kuijua imani sawasawa ni kuwa umegundua, yule mama
alikuwa na mambo mawili makubwa, kwanza alikuwa na msimamo pili alikuwa na uhakika
na anachokiomba majibu yake yapo. Uhakika ulimpa msimamo na msimamo
ulimsaidia kulinda imani na kupata alichokuwa anakihitaji.
Jambo
la ajabu, ni majibu ya Yesu, mstari wa 26 aliposema kuwa chakula alichonacho ni
kwa ajili ya watoto wake na siyo kwa ajili ya mbwa, kwa lugha nyingine alimuita
yule mama kuwa ni kama mbwa kwake. Hivi mfano wewe ukamwendea Yesu na kumsihi
ukimuomba, halafu akakujibu kuwa ana majibu ya maombi ya watoto wake tu na siyo
mbwa; unaweza ukafanyaje. kwa haraka haraka, inaweza ikawa ndio mwanzo na
mwisho habari zako na Yesu, maana kama umemwendea kwa kumsihi na ukitegemea
atakusaidia halafu bado ni Mungu, lakini anakupa majibu ambayo hata mpagani
mwanadamu asingekupa kama umemwendea kwa unyenyekevu kiasi hicho.
Lakini
hebu mtazame mama yule kwa unyenyekevu anamkaribia Yesu na kusema “ndiyo Bwana”
kisha akajenga hoja asiyoitegemea Yesu, ni kweli mimi ni mubwa na pengine
sistahili kula chakula ulichoandalia watoto wako, “ lakini hata mbwa hula
makombo yaangukayo mezani pa bwana zao” Yesu alishangaa sana, maneno ya mama
huyo yalikuwa na maana hii; kwa kuwa sistahili kula chakula ulichowaandalia
watoto wako kwa sababu mimi ni mbwa wako
na siyo mtoto wako, basi uniruhusu tu nile makombo yaliyoanguka mezani pako
maana hiyo ni haki yangu kama mbwa wako.
Hii
ndiyo imani halisi inayotakiwa kwa watu wa MUNGU, ni wazi kuwa hujawahi
kujibiwa kama huyu mama alivyojibiwa na alivyokatishwa tamaa na Yesu mwenyewe,
lakini kwa imani yake alisimama akasema nina hakika na ninatarajia kupokea kwa
namna yeyote. Na alipojenga msimamo huo Yesu akamtazama akasema Mama imani yako
ni kubwa, na iwe kwako kama utakavyo, akapona
binti yake tangu saa ile.
Ukisoma
kwa kutafakari, na kwa undani unagundua kuwa, Yesu hakumuombea Yule mama juu ya
mtoto wake, ila alimwambia iwe kwako kama
utakavyo. Hebu fikri kama yule mama angekuwa
anataka awe tajiri mimi nakuambia saa ile ile yule mama angekuwa tajiri. Si kwa
maombi sana kuwa alipata alichotaka ila kwa imani yake, maana kama ni kuomba
aliomba vizuri tena kwa unyenyekevu mkubwa; kama umesoma vema yale maombi ya
yule mama yalikuwa ya unyenyekevu sana kuliko ya kwako unayoyaomba, hebu
yatazame “akampazia sauti akisema,
unirehemu maana yake unihurumie Bwana, mwana wa Daudi, lakini Yesu
hakumjibu neno. Wanafunzi walipomtazama yule mama wakamhurumia na wao
wakamwendea Yesu wakamsaidia kuomba wakasema mwache aende zake, maana yake
mtendee ili aende zake maana anaendelea kupaza sauti. Bado Yesu hakujali maombi
ya mama yule hata kwa kubembelezwa na wanafunzi wake, na badala yake akwaambia
hakuja kwa ajili ya yule mama ila kwa wana wa Israeli waliopotea. Mama hakurudi
nyuma japo kwa maneno hayo ilimtosha kuishi hapohapo, ila ajabu kuu aliendelea
pamoja na kwamba Yeye hata kujibiwa hakujibiwa, ila wanafunzi walimsaidia ili
angalau ajibiwe, bado anajibiwa kuwa Yesu hakuja kwa ajili yake. kwa hiyo
ilimaanisha kuwa asitegemee kuwa anaweza kutendewa chochote kama anavyoomba, kama ni kuondoka aondoke tu. Yule mama baada ya kuambiwa
hivyo akasogea akamsujudu, kuonesha kuwa hata kama
hukuja kwa ajili yangu ila mimi nakuamini, alipomsujudu akaomba tena akisema,
Bwana unisaidie. Baada ya Yesu kuona huyu mama anang’ang’ania akasema maneno
magumu sana ambayo sasa yule mama kama si imani kubwa aliyokuwa nayo angekufulu palepale.
Swali
langu kwako ni hili; huyu mama ana utofauti gani na wewe? Je Yeye hakuwa
mwanadamu kama wewe? Je Yeye hakuwa na haja kama wewe ulivyo na haja? Na je umewahi kuomba
ukakatishwa taamaa angalau robo ya huyu mama? Umewahi kujibiwa majibu kama alivyojibiwa huyu mama?. kwa kujiuliza hivyo,
angalia imani yako, utagundua huna imani, na ndicho chanzo cha kutokupata kile
unachotakana kuomba.
Hebu
ngoja nikuambie jambo moja hapa la ajabu ili uone imani inavyofanya kazi kwa
mhitaji lakini pia kwa yule anayeombea. Mathayo 17:14-16 inaeleza kisa kimoja, “Nao
walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti akisema. Bwana
umurehemu mwanangu, kwa kuwa anakifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi
huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamlete kwa wanafunzi wako, wasiweze
kumponya.” Ukiendelea kusoma unaona Yesu akichukia kwa ajili ya yule
mtu, na juu ya wanafunzi wa Yesu kwa kuwa hawakuwa na imani. Ila alipomaliza
kuwasema aliamuru wamlete kwake kisha akakemea yule pepo akamtoka yule mtoto. Wanafunzi wake walipoona hivyo, hawakulidhika
wakamwendea mstari wa 19 “kisha wale wanafunzi wakamwende Yesu kwa
faragha wakasema mbona sisi hatukuweza kumtoa? 20 Yesu akawaambia, kwa sababu
ya upungufu wa imani yenu, kwa maana, amini, nawaambia, mkiwa na imani kiasi
cha punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ondoka hapa uende kule, nao
utaondoka; wala hakutakuwa neno lisilowezekana kwenu”
Naamini
umeona kazi ya imani na jinsi imani ilivyo, ila ukisoma sehemu nyingine
wanafunzi walipoambiwa hivyo waliomba waongezewe imani ndipo Yesu akawaambi
mngelikuwa na imani hata chembe ya haradali , kwa maana kuwa hawakuwa na imani
hata ndogo japo walikuwa ni wanafunzi wa Yesu na walikuwa wanamwamini Yesu.
Hapo unagundua kuwa imani ni zaidi ya kumwamini Yesu, lakini pia amesema hakutakuwa na neno lisilowezekana kwenu.
Unafikri kwa nini mambo mengi hayawezekani kwako, ni kwa sababu huna imani japo
unamwamini Mungu. Ni wazi kuwa ungekuwa unaweza ungeniuliza swali sasa hiyo
imani ya zaidi ya kumwamini Mungu iko je? na ndio unafanya je?. Roho mtakatifu
alijua kuwa utahitaji kujua na ameweka majibu ya maswali yako hapa chini. Ila
nakusihi sana
isiwe tu kusoma na kuelewa bali iwe kusoma na kutenda hicho unachogundua na
kukielewa.
Ukisoma
hapo kwenye mathayo 17 lakini mstari wa 21 umetoa majibu. “ lakini namna hii
haitoki ila kwa kusali na kuomba” hapo humaanisha kuwa namana hiyo ya imani
inayoweza kutoa nguvu za namna hiyo haiwezekani isipokuwa kwa kufunga na
kuomba. Maana yake ni kuwa kuna kiwango cha imani unachoweza kukipata kwa kuamini
na kufanya kile unachokiamini kiwe hakika na kutenda vile unavyoaamini, lakini
kiwango halisi cha imani hupatikana kwa kufunga na kuomba.
Hii
ni kwa sababu mwanadamu ana namna ya mwili sana kuliko namna ya roho na kwa
kweli hakuna mahali popota ambapo mwili unakubali na kumruhusu mtu kuwa na
imani hasa ya utendaji, hivyo kufunga maana yake ni kuutiisha mwili ili
kupandisha ile nafasi ya roho, hivyo kumfanya mtu kuwa na hali ya roho kuliko
ya mwili. Pia kufunga huko kunaudhoofisha mwili ambako kudhoofika huko huifanya
roho kuwa na nguvu.
Pia
kuomba hutifua au hunyanyu hali ya roho, au hunyanyua hali ya kimungu ndani ya
mtu, na hupunguza kasi ya mwili kufikri kimwili na kuifanya akili ikae kwa
namna ya roho ambapo ni rahisi sana kuwa na imani na kuona kuwa kila kitu kinawezekana
kwa Mungu, na kwa kuwa unakuwa kwa namna ya roho zaidi utasikia msukumo ambao
unakusukuma kufanya kile unachokiamini na unapofanya kwa kuwa unafanya kwa
uhakika lazima kitokee.
Mpendwa
katika Kristo, siraha ya imani ni siraha kubwa sana,
na wakati mwingine imekupasa kufanya mazoezi ya imani, hata pale ambapo watu
wote wanaona ni ngumu, wewe unawaambia inawezekana, pale akili yako
inapokuambia hapa ni ngumu unalazimisha ikubali kuwa inawezekana hata kama kwa jinsi ya kawaida haiwezekani.
Kikubwa
jitahidi kuamini, na kufanya kile unachokiamini kiwe kweli, yaani kama unaamini
Mungu anaweza katika jambo Fulani weka uhakika, na kisha lifanye ikiwa unomba
uambiwe omba ukijua nikimaliza kuomba nitakuwa nimepokea, na ukimaliza hata kama hujaona majibu anza kujiaminisha kuwa umepokea
taratibu taratibu utaanza kusikia amani moyoni na kuona lile jambo
likikamilika.
Mungu
wa mbinguni akujalie kujua vema siraha za ufalme wake ili uwe askari mwema na
mtetezi wa wokovu wako na kuujenga mwili wa Kristo. Hata hivyo ujue kuwa ziko
siraha nyingine kama siraha ya Neno, Siraha ya
Maombi, Siraha ya Wokovu. Hizo ndizo siraha kuu za ufalme wa Mungu. Na hata
siraha hiyo ya imani imeelezwa kwa ufupi hivyo endelea kusoma kwenye maanidiko
juu ya imani na vitabu vya Neno la Mungu, semina, mikutano, na zaidi shuhuda
mbalimbali. Maana imani chanzo chake ni kusikia ambako huja kwa Neno la Kristo.
Mungu wa mbinguni akujalie mema yote.
“mjue sana
Mungu ili uwe na amani”
Mwl: Goodluck Kazili